Watu wengi ambao hawajazama ndani ya biashara wana picha fulani ya kwamba biashara au ujasiriamali ni
sehemu bora ya wao kuwepo. Kwa wengine inaweza kuwa sehemu nzuri kuwepo lakini wengi wanahangaika
katika biashara mpaka wengine wanajikuta wanataka kuutoa uhai wao kabisa. Hilo linatokana na
stress/msongo wa mawazo unaotokana na biashara.
Jambo muhimu na la msingi unalotakiwa kufahamu ni kwamba kazi kubwa ya Mjasiriamali au
mfanyabiashara ni kutatua matatizo ya watu, na uwezo wako wa kutatua matatizo ndio utakaokuwezesha
kupata mafanikio, kila unavyotatua matatizo makubwa zaidi ndivyo unavyozidi kupata mafanikio makubwa.
Kwa hivyo mfanyabiashara akiamka jambo la kwanza analotakiwa kujiuliza ni kwamba “Leo nina matatizo
mangapi ya kuyatatua?” Na sio rahisi kwani kila ukiwa na matatizo mengi ndio msongo wa mawazo unavyoongezeka.
Kwa mfano nimewahi kukutana na msongo wa mawazo baada ya tovuti za wateja wetu zaidi ya 10
zilipodukuliwa (hacked). Hii ilinipa wakati mgumu sana kwani sikuwahi kukutana na hili tatizo kabla na pili
nilikuwa sijui nichukue hatua gani kutatua tatizo hili kwa kuwa ni jambo ambalo sikuwahi kufanya, Kwa hivyo
nilipata msongo wa mawazo wa hali ya juu. Lakini niliitisha kikao na wafanyakazi wangu kwa ajili ya kutafuta
suluhisho. Lakini kabla ya kutafuta suluhisho ilinibidi kuwapigia simu wenye tovuti kuwajulisha kuwa tovuti
zao zimedukuliwa kabla ya wao kutupigia sisi. Na tulifanikiwa kulitatua tatizo hili ndani ya masaa 24.
Na kila siku unajikuta una tatizo la kulitatua, na muda mwingine wafanyakazi wanapata matatizo unatakiwa
kuwasaidia, muda mwingine serikali inadai kodi au mwenye ofisi anadai kodi, kwa hiyo kuna mambo mengi
yanayotokea ndani ya biashara yako ambayo yanaleta msongo wa mawazo. Hivyo unatakiwa ujue jinsi ya
kudhibiti stress ulizonazo, kwa sababu kama haujatengeneza fomula nzuri ya kudhibiti stress zako unaweza
ukajikuta kuwa upo katika kitu ambacho kinatakiwa kikupe furaha lakini kinakutesa.
Kuna wafanyabiashara wengi ambao biashara zao zinawaingizia pesa lakini stress wanazoendana nazo hadi
kuingiza pesa ni kubwa mno, Muda wote wapo kwenye simu wakigombana na watu, ni jambo ambalo linawaumiza watu wengi sana.
Na kama wewe upo katika biashara na upo katika hali hiyo na unashindwa kudhibiti hali hiyo basi biashara haikufai.
Kwa hiyo nifuatilie kwa makini sana kwani nataka nikupe hatua ambazo unaweza ukazifata ili kudhibit
msongo wa mawazo katika biashara.
Kabla sijakwambia hatua hizo, kwanza nataka ufahamu kwamba stress/msongo wa mawazo sio kitu kibaya,
bali ni ishara ya kutokea kwa jambo/kitu ambayo kutokana na ishara hiyo unatakiwa kuchukua hatua ya
kukabiliana na hilo jambo au kukimbia. Kama utakabiliana nalo hapo stress itakuwa imekusukuma kuchukua
hatua na kama utaogopa kukabiliana nalo hapo stress itakuumiza na kusababisha matatizo zaidi.
Jinsi ya Kudhibiti Stress/ Msongo wa Mawazo
Hatua ya Kwanza
Ni kuielewa kuwa huo msongo wa mawazo unatokana na nini, Kwa hivyo chukua kalamu na karatasi
uandike, labda inatokana na kazi nyingi sana zimerundikana au kuna kazi ambayo ulitakiwa kuikamilisha
ndani ya muda fulani lakini muda unakaribia kufika na bado hujamaliza.
Ukishajua stress yako inatokana na nini, na ushaandika. Kwa mfano stress yako inatokana na kuwa una kazi
nyingi na unatakiwa kuzikamilisha ndani ya muda husika. Unachotakiwa kufanya ni kuandika kila kazi/project
na mwisho wake (lini inahitajika). Kwa mfano Kazi ya kwanza inatakiwa baada ya siku 5, kazi ya pili inatakiwa baada ya wiki 1.
Hatua ya Pili
Fanya kitu kimoja kwanza mpaka umalize ndipo uende katika kazi nyingine. Kwa mfano katika kazi ulizonazo
kuna kazi unayotakiwa kuikamilisha baada ya siku 5. Anza na hiyo kazi na usifanye kazi nyingine mpaka hiyo
ikamilike.
Hatua ya Tatu
Jiulize, Nifanye nini ili niweze kumaliza hii kazi/project haraka na nani ninaweza nikamtafuta ili anisaidie
nifanye hii project haraka. Muda mwingine unahitaji mtu wa ziada wa kukusaidia kutatua tatizo lillilopo,
usibebe mzigo peke yako, unaweza hata kumchukua mtu kwa kumlipa. Kwa mfano sisi (Dr Said na Timu
Yangu) tulipopata tatizo la website za wateja wetu kudukuliwa tulilazimika hata kuwalipa watu nje ya nchi ili
waweze kutusaidia kutatua tatizo hili.
Kama umejikuta kila mara unapata stress katika biashara yako basi wewe umekuwa unaendeshwa na watu.
Ili kuepuka hilo Tenga muda usiku au hata asubuhi mapema weka ratiba ya siku yako, kwamba leo nitafanya
hiki na hiki na usiruhusu mtu kuharibu ratiba yako labda kuwe na dharura kubwa iliyojitokeza. Kwa kufanya
hivyo itakusaidia sana kuweza kudhibiti msongo wa mawazo na kuendesha biashara Yako Vizuri.
Pia kama ungependa kujifunza Jinsi ya Kutumia Mtandao wa Facebook na Instagrama kunasa Wateja, basi
tumekuandalia Video inayoelezea Jinsi ya Kutumia Mtandao wa Facebook na Instagram kunasa Wateja.
Kuangalia video hiyo Bonyeza hapa.