Kama umeshajaribu kutangaza biashara, bidhaa au huduma unazotoa kwenye mtandao wa Facebook bila ya kupata wateja wengi basi nisikilize kwa makini sana kwani katika makala hii nitakuonyesha njia sahihi ya kutangaza kwenye mtandao wa Facebook kwa njia ambayo itakupatia wateja wengi kwenye biashara yako.
Wafanyabiashara wengi wanaonilalamikia wananambia kuwa kila wanapotangaza kwenye mtandao wa Facebook aidha huwa hawpati wateja kabisa au wakipata wanakuwa ni wachache mno.
Kama wewe ni mmoja wao basi hakikisha unazingatia maneno yaliokuwemo humu ndani.
Kabla sijakuonyesha hatua za kufuata nataka ufahamu makosa unayofanya yanayokusababishia kukosa wateja .
Makosa 7 Unayofanywa Katika Kutangaza Biashara Yako Katika Mtandao Wa Facebook
- Huna brand yako binafsi na unatangaza aina ya bidhaa au huduma ambayo maelfu ya watu wengine wanatangaza jambo ambalo linakuzamisha kwenye ushindani mkubwa.
- Huna mfumo wa mauzo ya mtandao (online marketing system) wenye kukusaidia kukufanyia mauzo kwa niaba yako.
- Huna kurasa ya biashara ya Facebook (Facebook Business Page) na hata kama unayo inatangaza brand ya kampuni nyengine.
- Hulengi kundi la watu maalum kwa ajili ya bidhaa au huduma unazoto toa. Badala yake unajaribu kuuza kwa kila mtu.
- Unakimbilia kuuza bidhaa badala ya kuanza kujenga uwaminifu kwa wateja wako watarajiwa.
- Unatangaza bidhaa badala ya kutangaza utatuzi wa matatizo ya wateja wako watarajiwa.
- Unatumia ma group ya Facebook kutangaza bidhaa zako badala ya kulipia matangazo.
Haya ndio makosa makubwa yanayofanywa na wajasariamali na wafanyabiashara wengi katika mtandao wa Facebook na kama wewe unahangaika kupata wateja wengi kupitia mtandao huo wa Facebook basi utakuwa unfanya mengi yao.
Hatua 7 Za Kufuata Kuweza Kutangaza na Kupata Wateja Wengi Kupitia Mtandao Wa Facebook
1: Jenga Brand Itakayopendwa na Wateja Wako
Kama unataka kujenga biashara ya uhakika yenye ushindani mdogo na yenye wafuasi wengi wanaopenda bidhaa na huduma unazotoa basi huna budi isipokuwa kujenga brand yenye kupendwa na kuaminiwa na watu.
Na hii haijalishi kama bidhaa au huduma unazouza ni zako binafsi au za kampuni nyengine au kama wewe ni mmiliki au ni promoter wa kampuni fulani brand yako itakutofautisha na washindani wako na utakuwa unavutia zaidi kwenye soko kuliko washindani wako.
Vitu vya kufanya kujenga brand yenye kupendwa na watu:
1: Tengeneza jina la brand lenye kukumbukwa:
Moja ya sifa za majina yanayokumbukwa ni kuwa na sauti ya kujirudia. Kwenye saikologia ili jambo hujulikana kwa jina la ‘phonological loop’.
Brand kama Coca-Cola, M&M na Palm Pilot ni baadhi ya mifano ya majina yenye sifa hizo.
Sifa nyengine ni kuwa na jina ambalo linataja utatuzi wa matatizo ya wateja wako watarajiwa kwa mfano Slim Secret (Siri ya Kukonda).
Au unaweza ukachagua jina lolote ulipendalo. Kama utawahudumia wateja wako vizuri na wakafurahishwa na huduma yako, brand yako itakuja kupata umaarufu kama ilivyokuwa kwa Apple, Microsoft na Google.
Unaweza wewe mwenye ukawa ndio brand yako.
Wahamasisaji wengi kama Tony Robbins, Brian Tracy na Les Brown wametumia majina yao kuwa ndio brand yao.
Kama wewe upo katika biashara ambayo ujuzi au taaluma yako inahitajika kupata wateja basi ni vizuri ukaji brand wewe kama wewe.
2: Tengeneza Nembo (Logo) ya Kufa Mtu Kuwakilisha Brand Yako
Nembo (Logo) itakusaidia kuwakilisha brand yako kwenye:
- Tovuti yako
- Kurasa zako za mitandao ya kijamii (Facebook, Twitter, Youtube n.k)
- Kadi ya biashara (business card)
- Mabango
- Fulana
- N.k
Sehemu nzuri za kutengenezewa logo za kisasa ni Upwork.
Upwork ni tovuti yenye wataalamu tofauti unaowalipa kwa kazi unayowapa.
Kuhakikisha unapata watu wazuri, angalia sampo za kazi zao na maoni (reviews) ya wateja waliyofanyiwa kazi nao.
Kama maoni yao mazuri basi mara nyingi utapata mtu mzuri.
Kama bajeti yako ni ndogo kuna tovuti nyengine inayofanana na Upwork iitwayo Fiverr ambayo wanatoa huduma tofauti ikiwemo ya kutengeneza logo kuanzia dola tano tu.
3: Tengeneza Tovuti
Tovuti ndio ofisi/nyumba yako kwenye mtandao.
Tovuti nzuri ni ile ambayo inamuonyesha msomaji ndani ya sekunde 5
- Wewe ni nani
- Unafanya nini
- Unawafanyia nani
- Wanatakiwa kufanya nini kunufaika na huduma yako
Vilevile tovuti nzuri ni ile yenye blogu kama hii utakayotumia kuwaelimisha wateja wako watarajiwa mara kwa mara.
Jiepushe na kutumia tovuti na blog za bure na badala yake sajili domain (yaani jina-la-tovuti-yako.com) na lipia urushaji wa tovuti yako (hosting)
Kama utapenda sisi tukusaidie kwa hilo unaweza ukatutumia ujumbe hapa.
Tuna OFA za kufa mtu katika vifurushi vyetu.
Kwa hivyo hakikisha unawasiliana nasi kabla hujamwaga pesa zako kwengine.
5: Waelimishe wateja wako watarajiwa mara kwa mara
Ili kujenga uaminifu kwa wateja wako watarajiwa basi hakikisha unaandika makala au kutengeneza video mara kwa mara yenye kuwaelimisha.
2: Tengeneza Smaku Ya Mtandao (Online Marketing System) Utakaokusaidia Kupata Wateja Wengi
Internet ni moja ya teknolojia bora kuliko teknolojia yoyote katika karne hii ya 21.
Na raha internet ni kuwa unaweza kutengeneza mifumo (systems) ya kukurahisishia kufanya vitu tofauti.
Moja ya mifume unayoweza kutengeneza kwa ajili ya kukuletea wateja ni Smaku Ya Mtandao.
Mjasiriamali yoyote asiyemiliki Smaku Ya Mtandao atakuwa hajaonja mataunda ya intaneti.
Smaku Ya Mtandao ni Nini?
Smaku Ya Mtandao ni mfumo wa masoko ya mtandao (online marketing system) unaotengenezwa kwa ajili ya:
- Kukusanya taarifa za wateja wako watarajiwa
- Kuwaelimisha
- Kujenga uaminifu na
- Kuuza bidhaa au huduma kwa niaba yako
Kujifunza zaidi kuhusu jinsi ya kutengeneza Smaku Yako Ya Mtandao bofya hapa
3: Tengeneza kurasa ya Biashara Ya Facebook
Katika mtandao wa Facebook kuna kurasa aina mbili:
- Kurasa binafsi na
- Kurasa ya biashara
Kurasa ya binafsi ni kwa ajili ya kujenga mahusiano na watu binafsi.
Hii ni kurasa ambayo unaitumia kuwasiliana na ndugu majamaa na marafiki.
Kurasa ya biashara ni kwa ajili ya biashara/brand yako na inatumika kujenga ukaribu na wateja wako watarajiwa.
Kosa kubwa watu wanalofanya ni kutumia kurasa zao binafsi kwa ajili ya biashara.
Kurasa zao zimejaa picha za bidhaa wanazouza na watu hawatambui uso wa mtu nyuma ya pazia ya kurasa ile.
Usiwe kama watu hao na uhakikishe unatenganisha kurasa yako binafsi (kwa ajili ya kuwasiliana na ndugu majamaa na marafiki) na kurasa yako ya biashara yenye kujenga ukaribu na wateja wako watarajiwa.
Faida nyengine kubwa ya kurasa ya biashara ni kuwa utaweza kufanya matangazo ya kulipia kama nitakavyokuonesha hapo chini.
4: Lenga Kundi la Watu Maalum
Mara nyingi akili zetu hutudanganya kuwa tukilenga watu wengi ndio tutauza sana na kutengeneza pesa nyingi.
Ingekuwa jambo hilo ni kweli basi madaktari wa kawaida (wanaotibu wagonjwa wa aina zote) wangekuwa wanalipwa mishahara mikubwa kuliko madaktari bingwa (wanaotibu wagonjwa wachache wa aina moja).
Kuna faida nyingi za kulenga kundi la aina moja ya watu. Baadhi yao ni:
- Utakuwa unawaelewa wateja wako vizuri sana kuliko washindani wako.
- Utakuwa na uwezo wa kuwapa bidhaa au huduma yenye kutatua matatizo ya wateja wako
- Utapata umaarufu haraka. Kumbuka! Daktari bingwa jopokuwa huhudumia wagonjwa wachache ni maarufu kuliko daktari wa kawaida.
- Kwa vile wewe utakuwa umebobea katika kuwasaidia wachache kwenye soko ujuzi na ubora wako utakuwa wa kiwango cha hali ya juu kuliko anayejaribu kuridhisha makundi mia ya watu.
Ndio maana mtaalamu mmoja wa masoko ya intaneti amesema,
If you want to be broke, target all the folks.
If you want to be rich, target a niche.
Yaani,
Ukitaka kufilisika, walenge watu wote.
Ukitaka kutajirika, lenga kundi la watu maalum.
5: Jenga Uaminifu Kwa Wateja Wako Watarajiwa Kwa Kuwaelimisha
Ukitaka wateja wako watarajiwa wakuchukie na waache kukufuata, tumia mtandao wa Facebook kutangaza bidhaa na huduma zako masaa 24.
Watakukimbia haraka kama anavyokimbiwa mgonjwa wa ukoma.
Ila kama unataka upate wafuasi wengi wanaokupenda, wanaokuheshimu na kukuamini basi hakikisha unawaelimisha wateja wako watarajiwa.
Moja ya misemo ya masoko ninayopenda sana ni kutoka kwa Perry Marshall anayesema,
Nobody who bought a drill wanted to buy a drill. They wanted to make holes.
If you want to sell drills do not advertise the drill. Advertise how to make holes.
Yaani,
Hakuna aliyenunua drili alitaka kununua drili. Alitaka kutoboa ukutu.
Kwa hivyo ukitaka kuuza drili usitangaze drili. Tangaza ‘jinsi ya kutoboa ukuta’.
Kama unauza cream ya bei nafuu ya kuondoa chunusi unaweza kuandika makala au kurekodi video yenye kichwa cha habari ifuatayo,
‘Njia 5 za Salama za Kuondoa Chunusi Kwa Gharama Ndogo’
kama unauza baiskeli za kupandia milima (mountain bikes) unaweza kuandika au kurekodi video
“Baiskeli Aina 7 Zinazosifika Kwa Kupanda Milima” au “Sababu 5 Kwa Nini Kila Kijana Wa Kitanzania Anatakiwa Kumiliki Mountain Bike”
Mwisho wa makala yako unaweza kutoa OFA kwa kusema kitu kama,
kama umependa makala hii naomba unisaidie kuisambaza kwa kubofya ‘share’ na kama ungemependa ku (andika utatuzi wa tatizo lake), tuna bidhaa tulokuwa nayo tunayotoa OFA kwa kipindi kifupi.
Kupata OFA hii piga simu namba 07XX – XXX XXX au Bofya hapa kuweka oda yako.
Makali hii ni vizuri ukayaandika katika blogu yako na kuisambaza katika kurasa yako ya Facebook.
Video ni vizuri ukairusha moja kwa moja kwenye kurasa yako ya Facebook ili iwafikie watu wengi na watizamaji wapate kuisambaza kiurahisi.
Mimi nimekuwepo katika soko kwa kipindi kirefu na ninakuhakikishia kuwa hakuna wateja watakaokupa heshima na kukuamini kama wale uliowaelimisha.
Hawakuoni kama mfanyabiashara, wanakuona kama mtaalamu mwenye nia safi ya kutatua matatizo yao jambo ambalo litakutofautisha katika yako na washindani wako.
Na japokuwa wengi wao hawatokuwa tayari kununua kutoka kwako papo hapo, wapo wengine watakuja kufanya hivyo baada ya miaka 3, 5 au hata 10.
Utapata wafuasi wengi na kuuza bidhaa nyingi.
6: Wafikie Maelfu Ya Watu Kwa Kulipia Matangazo Ya Facebook (Facebook Advertising)
Wafanyabiashara wengi wadogo wa kiTanzania na Afrika mashariki kwa ujumla wana uoga fulani wa kulipia matangazo.
Na uoga huu unatokana na dhana potofu ambayo ni…..
“Hatuna hela za kulipia matangazo.”
Jambo ambalo si kweli.
Nasema hivyo kwa sababu kulipia matangazo kwenye mtandao wa Facebook unaanzia gharama ndogo sana ($3 (Tsh. 7000) tu) gharama ambazo kila mfanyabiashara ana uwezo nao.
Na uzuri wa kutangaza Facebook ni kuwa una uwezo wa kuwalenga watu unaowataka walione tangazo.
Kama unauza bidhaa kwa wanawake na unataka tangazo lako lionekane na wanaweke wenye umri fulani na wanaishi katika mkoa fulani basi unaweza kufanya hivyo.
Hatua za Kuweka Tangazo Kwenye Mtandao Wa Facebook
1: Fuata hatua za Awali Nilizoziainisha Hapo Juu
Kabla ya kuweka tangazo ni vizuri ukahakikisha:
- Una brand yako tayari
- Unamiliki Smaku Ya Mtandao (muhimu sana ila sio lazima)
- Umeshatengeneza Kurasa ya biashara ya Facebook
- Umeshajua unataka kuwalenga nani
2: Nenda katika kurasa ya Facebook Ya Kuweka Matangazo na chaugua aina ya Tangazo Unalotaka Kuweka
Kuenda huko fuata linki ifuatayo https://www.facebook.com/ads/manager/creation/creation/
Au kama Facebook yako ipo kwa lugha ya kiswahili utaona hivi:
[Mimi nitaendelea kutumia Facebook English kwenye makala hii kwani kuna sehemu nyengine aidha haikutafsiriwa vizuri au haikutafsiriwa kabisa]
Baada ya kufika hapo ukiangalia kushoto kwako utagundua kuna hatua tatu unatakiwa kupitia kuweza kutengeneza tangazo lako:
- Campaign (Kampeni): lengo kuu la tangazo lako k.f kupata wateja kwenye duka lako.
- Ad sets (Seti ya Tangazo): Hizi ni seti za matangazo ya kampeni ile ile yenye kulenga watu tofauti kutokona na umri, sifa au jinsia. Seti tofauti zitakujulisha ni watu aina gani wanavutiwa zaidi na tangazo lako.
- Ad (Tangazo): Hili ndilo tangazo lenyewe kama watakavyoona wateja wako watarajiwa. Ni vizuri kujaribu matangazo tofauti kujua tangazo lipi linawavutia zaidi wateja wako watarajiwa.
Hatua ya 1: Chagua aina ya kampeni ya Tangazo unalotaka kuweka.
- Brand Awareness: Kwa ajili ya kufanya brand yako ijulikane (ni nzuri kwa makampuni makubwa yenye kutegemea utangazaji wa brand yao)
- Reach: Kwa ajili ya kuwafikia watu wengi kwa gharama ndogo yao katika maeneo ya biashara au ofisi yako
- Traffic: Kwa ajili ya kuwapeleka watu nje ya Facebook. Hii ni nzuri kwa wanaomiliki blogu na wanataka kupata wasomaji kwenye blogu zao.
- Engagement: Hii kwa ajili ya kupata ushiriki wa watu kwenye post zako za Facebook. Aidha unataka ‘likes’ , ‘comments’ au ‘shares’ ziongezeke.
- App Installs: Hii kwa ajili ya wanaotengezeza application za simu na wanataka zishushwe na watu wengi.
- Video views: Hii kwa ajili ya kupata watazamaji wengi wa video utakayorusha kwenye tovuti ya Facebook.
- Lead generation: Hii ni kwa ajili ya kujenga listi (majina, barua pepe na namba za simu) ya wateja wako watarajiwa.
- Conversion: Hii kwa ajili ya kupata watu watakaochukua hatua fulani baada ya kufika kwenye tovuti yako kwa mfano kuweka taarifa zao au kununua bidhaa.
- Product catalogue Sales: Aina ya tangazo hili litakuwa linaonesha listi ya bidhaa zako na bei zake kwa ajili ya kuwauzia wateja wako watarajiwa.
- Store visits: Hii kwa ajili ya kupata watu kuja dukani kwako. Kama una duka, aina ya tangazo hili litakufaa sana.
Elewa kuwa Facebook wanaongoza kuwa na takwimu za watu kuliko kampuni yoyote.
Wanajua
- watu gani wanapenda ku ‘like’ na ku ‘share’
- watu gani wanapenda ku bofya linki na kusoma makala
- watu gani wanapenda kununua bidhaa kwenye mtandao
- watu gani wanapenda kununua bidhaa kwenye maduka
- n.k
Ukiwaambia Facebook kuwa unataka wateja wa kununua bidhaa zako dukani, watahakikisha tangazo lako linaonekana mbele za macho ya watu wenye sifa ya kununua bidhaa madukani.
Kwa hivyo kuna umuhimu sana kuelewa kampeni gani italeta tija kwenye biashara yako.
Kwa makala hii nitachagua kampeni ya Traffic kupata wasomaji kwenye makala yetu ya Jinsi Ya Kuongeza Kipato Kutoka Kwa Wateja Wachache. .
Wewe hakikisha unachagua aina ya kampeni inayoendana na biashara yako.
Baada ya kuchagua kampeni ya Traffic, tunga jina la kampeni yako na bofya Continue.
Mimi yangu nimeiita “Traffic – Ongeza Kipato Wateja Wachache”
Baada ya kubofya continue, tunaingia katika hatua ya pili ambayo ni…..
Hatua ya 2: Chagua Seti (Ad Set) Ya Tangazo Lako
- Chagua jina la seti la tangazo lako. Kwa vile wateja wangu ni wafanyabiashara, mimi nimelitungia jina la Wafanyabiashara wa Dar es Salaam kwenye seti la tangazo hili.
- Chagua wapi unataka traffic yako iende. Kwa vile tunataka wasomaji wa blog yetu waongezeke, nimechagua Website or Messenger. Kama umetengeneza application ya simu na unataka watu waone app yako utachagua app.
- Chagua nchi au mkoa. Mimi nimechagua Dar es Salaam
- Chagua umri (mimi nimechagua umri kati ya 25 hadi 65 ndio umri wa wajasiriamali wengi)
- Chagua jinsia (mimi nimechagua wanaume pamoja na wanawake). Kama bidhaa yako inalengea jinsia moja basi chagua jinsia hiyo
- Chagua lugha (mimi nimechagua kiswahili kwani sitaki mtu asiyezungumza kiswahili kuona tangazo langu)
- Chagua vitu ambavyo unahisi wateja wako watarajiwa watavipenda. Kwa vile mimi nalenga wafanyabiashara nimechagua vitu kama matangazo, matangazo ya Facebook, promotion n.k.
- Chagua wapi unataka tangazo lako lionekane. Kuna sehemu tatu kubwa tangazo lako litaonekana; Facebook, Instagram na Audience Network (mtandao wa tovuti na application za simu). Hapa ni vizuri ukawacha automatic kama ni mgeni katika kutangaza Facebook.
- Weka bajeti ya tangazo lako. Hakikisha unaanza na bajeti ndogo ya dola $5 kupata kuona tangazo linaendelea vipi kabla hujatoa maamuzi ya kuongeza bajeti.
- Bofya Continue.
Hatua ya 3: Bandika Tangazo Lako
Bandika tangazo lako kwa kufanya yafuatayo,
- Tunga jina la tangazo
- Chagua kurasa ya biashara ya Facebook
- Chagua kurasa ya Instagram
- Chagua muundo wa tangazo lako (kama ni video, picha moja, picha nyingi au slaidi). Mimi nimechagua single image (picha moja).
- Chagua picha. [Hakikisha picha hiyo ipo katika miraba ya pixel 1200 X 628]. Unaweza ku design picha nzuri za matangazo kwenye tovuti ya Canva.
- Weka linki ya tovuti yako
- Weka kichwa cha habari ya tangazo lako. (Kwa vile tangazo langu lilikuwa ni makala nimeweka kichwa cha habari ya makala.)
- Weka maandishi ya post yako.
- Chagua maandishi ya kitufe. Mimi nimechagua learn more (soma zaidi).
- Weka maelezo ya ziada ya tangazo lako. Maelezo haya huonekana chini ya kichwa cha habari.
- Andika linki unvyotaka ionekane kwa wateja wako watarajiwa.
- Weka oda kwa kubofya ‘Place Order‘.
Baada ya hapo subiri Facebook wahakiki tangazo lako kabla ya kurushwa hewani.
Japokuwa mfano huu niliotumia ni kwa kupata wasomaji wengi katika makala yangu, wewe unaweza kuchagua kampeni inayoendana na biashara yako.
Mimi hupenda kuwaelimisha wasomaji wangu kabla sijatoa OFA yoyote.
Na kwa vile tumezungumzia OFA nina video nimekuandalia yenye kukuonyesha Jinsi Ya Kutumia Mtandao Kunasa Wateja kama Smaku.
Ndani ya video hiyo nimeongelea mambo 3 ya lazima kila mfanyabiashara anatakiwa kufanya kuweza kunasa wateja kama smaku.
Kama unataka kujua zaidi bofya hapa.
Kabla hujaondoka naomba unijulishe changamoto unazokutana nazo katika kutangaza bidhaa au huduma zako Facebook.
Na kama umependa makala hii basi nisaidie kusambaza Facebook, WhatsApp na mitandao mengine kwa kubofya vitufe husika hapo chini.
Asante sana kwa kusoma makala hii ndefu.
Ni mimi mwenye kujali mafanikio yako,
Dr. Said Said
1 Response to "Jinsi Ya Kutangaza na Kupata Wateja Wengi Kupitia Mtandao Wa Facebook"
[…] M ya 3 ni Message (ujumbe). Wengi vile vile wanakosea katika kuandika ujumbe wa matangazo yao. Wanazungumzia sana kuhusu bidhaa/huduma wanayotoa badala ya kuzungumzia matatizo ya wateja wao watarajiwa na kuwaahidi namna ya kutatua matatizo hayo. Nimekoleza neno kuwaahadi kwa sababu tangazo linatakiwa kutoa ahadi ya kutatua tatizo la wateja wako watarajiwa na sio kuuza bidhaa (isipokuwa kwa kesi maalum). Ngoja nikuonyeshe mfano: Hili ni moja ya tangazo lilopokewa vizuri sana na watu. Kwa $14 tumeweza kukusanya taarifa (majina na email) za watu zaidi ya 200. Tangazo hili lilionekana Facebook na Instagram na tulikuwa tunawakaribisha watu kuhudhuria darasa live lenye kufundisha “Jinsi Ya Kutumia Mtandao Kunasa Wateja Kama Smaku“ Hebu tulichambue hili tangazo: Kipengele cha kwanza: Je wewe ni mfanyabiashara au mjasirimali unaehangaika kupata wateja kupitia mtandao? Kama unavyoona, nimeanza na swali linalolowagusa wateja wangu watarajiwa. Kama anayesoma si mhusika, sina mpango nae. Kipengele cha pili: Kama ndio basi usihofu kwani Dr. Said Said, Mkurugenzi wa kampuni ya Online Profits ameandaa darasa bure kwenye mtandao ambayo utajifunza “Jinsi ya kutumia mtandao wa intaneti kunasa wateja kama SMAKU“ Ikisha nimejaribu kujenga uaminifu kwa kujitambulisha kwa jina na cheo changu. Kipengele hiki ni muhimu kwani inawaonyesha wateja wako wewe ni nani na kwanini wanatakiwa kukusikiliza. Kipengele cha tatu: Katika darasa hili utagundua yafuatayo: 1. Kwa nini wajasiriamali wengi wanashindwa kupata wateja kupitia mtandao 2. Siri ya kupata wateja wengi wenye hamu ya kununua bidhaa au huduma unayotoa 3. Mfumo wa mtandao pekee wenye uhakika wa kukuletea wateja wengi kuliko kitu chochote Nimewaambia watapata nini wakibofya linki. Kumbuka, lengo ni kutoa sio kuuza. Kipengele cha nne: Nenda hapa kujisajili >> Jinsi Ya Kutumia Mtandao Kunasa Wateja Kama Smaku – Online Profits Muda unakimbia na siti ni chache. Jisajili sasa hivi kwa kuenda hapa>> https://goo.gl/rMc3Lk Nimewapa linki na kuwahimiza kwanini wanatakiwa kuchukua hatua mara moja na kutosubiri baadae. Bila ya kufanya hivyo wapo watakaopuuza na kusema nitafanya baadae. Na formula hiyo huwa naitumia takriban katika matangazo yangu yote. Kama unataka kujifunza kiundani hatua kwa hatua nimeenda wapi kwenye mtandao wa Facebook kuandaa hilo tangazo, unaweza kusoma makala ya “Jinsi Ya Kutangaza na Kupata Wateja Wengi Kupitia Mtandao Wa Facebook“ […]