Kama wewe ni mjasiriamali au mfanyabiashara unaehangaika kupata wateja kutokana na ushindani basi naomba unisikilize kwa umakini sana, kwani katika makala hii nataka nikuonyeshe mbinu ambayo itakusaidia:-

  1. Kuua ushindani kwenye soko lako na
  2. Kuwafanya wateja wavutiwe kuja kununua bidhaa/huduma unayotoa kutoka kwako badala ya washindani wako.

[Bofya hapa ku Subscribe kwenye Channel yangu]

Mbinu hii nimejifunza kwenye kitabu kiitwacho Blue Ocean Stratagy (Stratejia za Bahari ya Bluu) iliyoandikwa na Chan Kim.

Ndani ya kitabu hicho anazungumza stratejia za aina mbili:

  1. Red Ocean (yenye kufatwa na 90% ya wajasiriamali wanaohangaika) na
  2. Blue Ocean (yenye kufuatwa na wachache wenye kuteka soko)

Tofauti ya stretejia (mbinu) hizi mbili inatokana na mfano ambao ametoa wa mapapa wenye kutafuta samaki.

Anasema mfanyabiashara ni kama papa mwenye kutafuta eneo lenye samaki samaki kwa ajili ya kula. Na samaki ni mteja wa mfanyabiashara yule.

Papa huyo akigundua eneo lenye samaki na kuanza kula wale samaki, baada ya muda fulani atapita papa mwengine kuja kula samaki katika eneo lile.

Na baada ya muda atakuja mwengine na mwengine hadi itafika wakati papa hao wanakuwa wengi kuliko idadi ya samaki na wanashtukizia kuwa wanatafunana wenyewe kwa wenyewe hadi damu kumwagika na kufanya rangi ya ile bahari kuwa nyekundu, na ndio maana ikaitwa red ocean strategy.

Huo ndio mfano wa wafanyabiashara wengi.

Utakuta mtu anaanzisha duka lake. Mambo yake yanaenda vizuri na anaanza kupata wateja.

Mtu mwengine anaona ile biashara na kusema “Kumbe biashara ile inalipa! Wacha na mimi nianzishe duka langu.”,

Anaanzisha duka lake na kuingia kwenye ushindani na yule aliyefungua duka la mwanzo. Baada ya muda, mwengine nae anaanzisha duka lake na kuingia kwenye ushindani na wale wawili.

Inafika wakati mlolongo wa watu wanafungua biashara kama ile na wanaingia katika ushindani hadi wanafikia 20, 30 hali ya kuwa idadi ya wateja bado ni ileile.

Inafika wakati wanajikuta wapo katika ushindani na biashara zote zinakuwa zinaumia.

Lakini Blue Ocean Strategy inakufanya wewe kujichomoa katika eneo lile la bahari na kuenda katika eneo jengine ambalo halina mapapa na kuwavuta samaki kuja kwako.

Na kwa vile lile eneo ni lako na ushaweka bendera yako hata papa mwengine akija hawezi kushindana na wewe kwa sababu eneo lile unalifahamu vizuri na samaki wale wamevutiwa na wewe kuliko mapapa wengine.

Vipi unaanzisha Blue Ocean Strategy?

Kwanza unatakiwa kufahamu kuwa kuna aina mbili za wajasiriamali au wafanyabiashara ambao ni

  1. Generalist na
  2. Specialist

Generalist ni mfanyabiashara anayewalenga wateja wote na Specialist ni mfanyabiashara anayelenga kundi fulani tu la watu na anafanya hivyo kwa sababu anajuwa kuwa hakuna mtu mwengine kama yeye anayeweza kutatua matatizo ya kikundi hilo kama yeye.

Ingawa watu wengi wanaona ni bora kuwa generalist kwa sababu soko lake ni kubwa, kitu wasichokifahamu kuwa kuwa generalist haitaji taaluma kubwa na soko lenye taalum ndogo linakuwa na ushindani mkubwa kuliko soko lenye taaluma ndogo.

Lakini ukiwa specialist unakuwa na uwezo wa kuwanasa watu wengi kwa sababu wewe unaonekana kuwa ni mtaalamu mbele ya macho ya soko lako na watu wanakufata wewe na wapo tayari kukulipa pesa zaidi kuliko yule mtu ambaye anaonekana anafanya kila kitu (generalist).

Na mfano mzuri ni kama madaktari.

Daktari ambaye anatibu wagonjwa wote ni generalist (MD) na daktari ambaye ni specialist anaona wagonjwa wachache lakini analipwa pesa nyingi na super specialist analipwa pesa nyingi zaidi kuliko wote.

Na kama wewe unataka kuua soko lako basi huna budi kuwa specialist au hata super specialist.

Mfano mimi (Dr Said) nilivyoanza biashara yangu niliingia katika soko la web design ambalo lilikuwa na ushindani mkubwa.

Nilianza kuwatengenezea tovuti wafanyabiashara, lakini nikaona nikijiweka kama Web Designer watu watanifananisha na Web Designer wengine na kunihoji kuhusu bei zangu kuwa juu kulinganisha na web designers wengine.

Hivyo sikujiweka kama Web Designer, na hata nilipokuwa nawapigia simu nilikuwa nikiwaambia

Hello! Kwa jina naitwa Dr. Said Said, ninawasaidia wafanyabiashara kama wewe kutumia tovuti kunasa wateja kwenye mtandao. Na sasa hivi natoa consultation ya bure ya saa 1. Je ungependa kupata consultation ya bure kujifunza namna unavyoweza kutumia tovuti yako kunasa wateja?

Wengi walikuwa wanajibu kuwa wangependa kupata consultation hiyo.

Na mimi nikienda kule nawaonyesha njia wanazoweza kutumia kupata wateja kwenye biashara zao kupitia website (tovuti) na sio jinsi wanavyoweza kumiliki website yenye kupendeza.

Najua wateja wangu hawajali sana kuhusu kumiliki website nzuri kama wanavyojali kupata wateja kupitia website zao.

Kujiweka kwangu kama Specialist (Online Marketer) kumenisaidia sana kupata projects nyingi zenye thamani (Blue Ocean Strategy) badala ya kujitangaza kama web Designer ambayo ni Red Ocean fani yenye ushindani mkubwa.

Mbinu hiyo na wewe unaweza kuitumia katika biashara yoyote ile.

Tuchukulie mfano wa biashara ya tour:

Muda si mrefu nimetoka kupigiwa simu na mmiliki wa kampuni ya tour na anataka ushauri vipi aitumie website yake kupata wateja.

Kitu cha mwanzo nilichomwambia ni kujiposition vizuri kwenye soko kama specialist badala ya generalist, ushauri huohuo ambao niliokupa wewe nilimpa yeye.

Badala ya kusema sisi ni tour company ambao tunapokea wageni kutoka nje sema sisi tunaspecialise kuwasaidia kundi fulani la watu kupata jambo fulani.

Kwa mfano nina rafiki yangu ambaye yeye amejikita kwenye motorbike safari.

Anasema “Sisi tunashughulika na Adventure safari za Motorbike tu! Kama wewe hujui kuendesha pikipiki hapa sio kwako”.

Kwa haraka haraka unaweza kuona kuwa atapata wateja wachache lakini kwa vile hana ushindani, wateja anaowapata wanamtosha sana na anatengeneza pesa nzuri sana na anaweza kuweka chaji ambayo washindani wake hawawezi kuweka kwa sababu washindani wake hawafanyi motorbike safari.

Swali unalotakiwa kujiuliza nia nijiweke vipi kwenye soko kama mtaalam wa kitu fulani ili niwavute watu waje kwangu?

Siku zote angalia wateja wako wana matatizo gani na kitu gani maalumu utafanya.

Usijaribu kufanya mambo mengi . Chagua kitu kimoja tu cha kufanya.

Muhimu hilo tatizo liwepo katika soko na watu wachache waweze kutatua hilo tatizo. Kama wewe ni miongoni mwa hao wachache ambao wanaweza kutatua tatizo hilo basi nakuhakikishia utapata wateja wengi na utakuwa huna ushindani katika biashara yako.

Ifanyie kazi na unijulishe umefaidika vipi na mbinu hiyo.

Kama umependa makala hii basi utapenda video yangu niliyotengeneza yenye kukuonyesha Jinsi ya Kutumia Mtandao wa Facebook na Instagram Kunasa Wateja (Bofya hapa).

Usisahau ku ‘share’ hii makala Facebook kwa kubofya kitufe cha Facebook hapo chini ili na wengine wafaidike.

Ni mimi mwenye kujali mafanikio yako,

Dr. Said Said
Mkurugenzi wa Online Profits


Ujumbe Wa Facebook

Leave a Reply

Your email address will not be published.