Kama wewe ni mfanyabiashara au mjasiriamali unayehangaika kukuza biashara yako basi ukifanya njia tatu hizi huenda mambo yakabadilika kwa kiasi kikubwa sana:
1. Ongeza Idadi Ya Wateja (Increase the Number of Customers)
Nafikiria unafahamu kuwa wateja ndio wanaokuingizia pesa katika biashara yako.
Na kila ukiwa na wateja wengi ndivyo kipato kinavyozidi.
Na kila wanavopungua ndivyo kipato kinapungua na hatimae kuuwa biashara yako.
Je Wateja Wako Utawapata Wapi?
Wateja hawapatikani isipokuwa wewe (au hata watu wengine) kutangaza kwa watu kuwa una biashara fulani yenye kutoa bidhaa au huduma fulani.
Na njia kuu ya kupata wateja ni kutangaza.
Na matangazo unaweza kufanya kwa njia mbili.
- BURE – Kuwa na duka au ofisi sehemu iliyo mbele za nyuso za watu, kuongea na watu ana kwa ana, kutumia mitandao ya kijamii n.k
- Kulipia matangazo – Hii itakusaidia kuwafikia maelfu ya watu kwa mpigo kitu ambacho kitakusaidia kuongeza idadi ya wateja wapya mara moja.
Japokuwa njia hii ya kwanza ni muhimu kwa kila biashara, njia hii huwa haitoshelezi hususan kama unatumia gharama kupata hao wateja kwani unaweza ukajikuta pesa unazotumia katika matangazo ni sawa au makubwa kuliko faida unayopata katika mauzo, na ndio maana unahitaji ku…..
2. Ongeza Idadi Ya Mauzo Ya Kila Mteja (Increase the Unit of Sales)
Kama kila mteja anakuingizia wastani wa shilingi elfu kumi kwa kila manunuzi, inabidi ujitahidi kumshawishi mteja huyo kununua bidhaa za ziada zitakazokufanya uongeza mapato kwa kila manunuzi.
Swala la kujiuliza ni bidhaa gani ya ziada unayoweza kuwauzia wateja wako juu ya kile kitu wanachonunu kila siku?
Kama wewe upo katika biashara ya kuwatengenezea wateja wako tovuti, basi watahitaji kusajiliwa domain name na kurushiwa tovuti yao hewani au watahitaji kutengenezewa logo.
Kwa hivyo badala ya kumuuzia huduma ya kuwatengenezea tovuti ambayo pengine itakuingizia $500 peke yake, unaweza ukaingiza $20 ya usajili wa jina la tovuti hilo na $160 ya urushaji na $50 ya logo.
Kwa hivyo badala ya kuingiza $500 kwa kila mteja utakuwa unaingiza $730.
Na uzuri ni kuwa haikugharimu pesa yoyote kuongeza kipato hicho.
Na hii unaweza kufanya katika biashara yoyote hata kama una kiduka kidogo cha kuuza vitu vya kuhitajika majumbani.
Kwa mfano ukiuza siagi unaweza kutoa ofa kwa mteja wako anunue na jam kwa bei pungufu.
KFC na McDonalds ni mahodari sana katika hili.
Ukiweka oda ya burger, wanakuuliza “je utapenda tukuwekee na chipsi katika hiyo burger?” ukisema ndio wanakuuliza tena “utapenda tukuwekee na kinywaji gani?”
Wewe na yako ilikuwa ni burger pekee yake lakini umejikuta unanunua na chipsi na soda.
3. Ongeza Idadi Ya Mauzo Endelevu (Increase the Frequency of Sales)
Jambo la tatu la muhimu kufanya ni kuhakikisha wateja wako wanarudi kwako mara kwa mara kununua bidhaa au huduma unayotoa.
Unaweza kufanya hivi kwa:
- Kuuza bidhaa au huduma inayopendwa na wateja wako
- Kuwasiliana na wateja wako mara kwa mara kuwajulisha kuhusu OFA au bidhaa au huduma mpya unayotoa.
Hizo ndizo njia 3 pekee za kufanya kukuza biashara yako.
Je wewe unafanya njia ngapi?
Tujulishe kwa ku ‘comment’ hapo chini bila ya kusahau ku bofya ‘share’ ili na wengine wengi wafaidike.
Wako,
Dr. Said Said