Kama wewe ni mjasiriamali mwenye bidhaa au huduma nzuri lakini unashindwa kuwafikia watu wengi kwenye mtandao basi hakikisha unanipa macho na masikio yako kwani huenda makala hii ikawa moja ya makala muhimu utakayosoma mwaka huu.
Kutokana na uzoefu wangu wa kutumia mtandao kwa miaka zaidi ya 6 kupata wateja, nimegundua kuna mambo 5 ukiyafanya vizuri basi utawafikia watu wengi na kuuza bidhaa nyingi sana.
Mambo yenyewe ni:
1. Zingatia Ubora:
Ukiwa unatoa bidhaa au huduma nzuri kwenye soko yenye kutatua matatizo ya wateja wako, basi utapata majeshi ya watu watakaokusaidia kusambaza ujumbe kuhusu bidhaa yako bila ya wewe kuwalipa chochote.
Wajasiriamali wa Silicon Valley, Marekani wana msemo wao unaosema,
The goal is to develop a product so good that customers will move the products for us before we consider marketing it.
Yaani,
Lengo ni kutengeneza bidhaa nzuri sana kiasi ambacho wateja wetu watatutangazia kwenye soko kabla ya sisi kufikiria kuitangaza wenyewe.
Na moja kati ya sifa muhimu wawekezaji wa makumpuni ya Silicon Valley (akina Facebook) wanaangali ni bidhaa nzuri zinazoweza kutangazwa na watumiaji?
2. Kuwa Tofauti
Ukiwa tofauti unakumbukwa.
Moja ya kosa kubwa linalofanywa na wafanyabiashara wetu ni kuangalia washindani wako wanafanya nini na kuwaiga.
Ukifanya hivyo basi usitegemee biashara yako kudumu miaka mingi.
Kuwa mbunifu na jiweke tofauti kabisa na washindani wako.
Mfano mzuri ni kampuni ya viatu iitwayo Vibram Five fingers, viatu vilivyokaa kama glovu za mikono.
Walipoviingiza viatu vyao sokoni vilianza kuenea kama virusi vya flu na kila aliyekuwa anaviona viatu hivyo alikuwa akivitamani.
Kwa nini? Mbali na bidhaa yao kuwa nzuri, walikuwa tofauti kabisa na viatu vyengine.
Ukiwa tofauti utakumbukwa siku zote.
Hutafananishwa na mamia ya washindani wako wanaofanana.
Na kila ikiwa rahisi kukumbukwa inakuwa ni rahisi vile vile kuwafikia watu wengi.
3. Toa Kabla Hujapokea
Japokuwa umeanzisha biashara yako kutengeneza pesa, jiulize kitu gani unaweza kutoa BURE kabla ya kuuza bidhaa yoyote?
Hii ni muhimu sana kwani wateja wako watarajiwa hawakujui, hawakupendi na wala hawakuamini.
Kwa hivyo ukiwazawadia kitu chochote, utajenga uaminifu kwa urahisi na kwa kasi kubwa sana hususan katika mtandao.
Vitu unavyoweza kutoa ni kama:
- Ushauri
- Sampuli ya bidhaa
- Mafunzo (kama haya ninaokupa mimi)
- N.k. (Kuwa mbunifu)
Lengo la utoaji ni kuwaonesha wateja wako watarajiwa kuwa hupo pale kula pesa zao bali unawajali na unataka bidhaa / huduma unayotoa iwasaidie kutatua matatizo yao.
4. Tengeneza Smaku Ya Kunasa Wateja Kwenye Mtandao
Watu wengi nikiwaambia hili hawaamini kuwa ni jambo linalowezekana lakini kwa dunia ya sasa amini usiamini ni jambo ambalo mtu yoyote anaweza kufanya hata kama hana elimu ya kompyuta.
Hii ni topic ndefu kidogo ila kama unataka kujifunza zaidi nimetengeneza video yenye kueleza namna ya kufanya hivyo hapa.
5. Tangaza! Tangaza! Tangaza!
Matangazo ni kama petroli kwenye gari lako.
Ukiacha kutangaza biashara yako haisogei mbele. Inakwama au inarudi nyuma.
Kwa vile washindani wamekuwa wengi kutangaza si jambo la hiari.
Ila ni muhimu kuzingatia matunda unayopata kutokana na kila tangazo uweze kuboresha na yazidi kukuletea faida.
Lengo ni kuwekeza pesa yenye kukusaidia kuleta mauzo yenye faida kubwa kuliko gharama za matangazo yako na kuendelea kufanya hivyo kila siku ili biashara yako ikuwe.
Ukiwa na mfumo mzuri kwenye biashara yako (ya mtandaoni na nje ya mtandao) kazi yako kubwa itakuwa ni
- Kutangaza na
- Kuboresha bidhaa na huduma zako
Natumai umefaidika na makala hii.
Nijuulishe kwa ku comment hapo chini, njia zipi unazotumia kwenye mtandao kuwafikia wateja wako.
Kama umefaidika na makala haya naomba unisaidie kusambaza Facebook, Twitter, Facebook na WhatsApp kwa kubofya vitufe husika hapo chini.
Wako,
Dr. Said Said