Kama unaendesha biashara yako na umefikia hatua ambayo unahisi umekwama au umekutana na kizuizi cha aina yoyote na unashindwa kuikuza biashara yako basi formula hii itakusaidia sana.

Na fomula hii nimejifunza kutoka kwa mtaalamu na hodari wa mambo ya masoko (Marketing Professional), Joe Polish

Na hii ndiyo fomula ambayo Bwana Joe Polish anawafundisha watu wanaomiliki makampuni makubwa duniani na kuwasaidia kutoka katika kampuni ndogo hadi kuwa kampuni kubwa.

Fomula hii inasema…

“More money is made when there is match between Opportunity and Capability”

yaani

“Pesa nyingi hutengenezwa kama kuna upatano au ulingano kati ya fursa na uwezo”.

Hii ina maana kwamba ili pesa itengenezwe kwa wingi ni lazima vitu viwili; Fursa na Uwezo wa kuzalisha Pesa viende sambamba.

Kama fursa ya biashara ipo lakini uwezo wa kutengeneza pesa ni mdogo mtu huwezi kutengeneza pesa za kutosha.

Vilevile kama uwezo unao lakini eneo ulilopo halina fursa basi hauwezi kutengeneza pesa nyingi.

Chukulia mfano wewe ni mtaalamu wa Upasuaji na Kutumia plastiki (plastic surgery) katika kuwapamba watu.

Ukijaribu kutumia taaluma yako katika nchi kama Tanzania utapata ugumu wa kutengeneza pesa kwani fursa ya soko lake sio kubwa.

Uwezo unao lakini fursa haipo.

Hii ndio changamoto kubwa ambayo wafanyabiashara wengi wanayo.

Wanaingia katika biashara yenye fursa kubwa lakini uwezo wa kukidhi mahitaji ya wateja wao ni mdogo. Ndio unakuta biashara inafika kikomo.

Mfano mzuri ni biashara ya utalii.

Makampuni mengi ya Utalii mkoani Arusha na sehemu nyenginezo kama Zanzibar yanahangaika na mwishoe kudai kwamba kuna ushindani ni mkubwa.

Lakini ukiangalia uhalisia wa mambo, si kweli kwamba ushindani ni mkubwa bali ni kwamba makampuni mengi hayana uwezo wa kutoa huduma nzuri inayoendana na fursa iliyopo.

Hivyo fursa ya utalii ipo lakini wengi wao hawana uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko lao.

Hivyo basi siku zote katika biashara yako kama umefika hatua umekwama jiulize, Je katika biashara ninayofanya fursa ipo au hakuna?

Kama wapo wafanyabiashara wengine wanafanya biashara kama yako na wanatengeneza pesa inamaanisha kuwa fursa hiyo ipo.

Baada ya kufahamu kwamba fursa ipo, sasa jiulize…

Nifanye nini ili niweze kuendana na fursa iliyopo katika soko?

Inawezekana ikawa unahitaji kumwajiri mtu mwingine mwenye uwezo mzuri katika masoko ambaye anaweza kukusaidia kuziwakilisha bidhaa zako vizuri katika soko.

Au inawezekana unahitaji kujifunza Jinsi ya Kutumia Facebook na Instagram Kunasa Wateja.

Fanya unachotakiwa kufanya kuboresha uwezo wako uendane na fursa iliyopo.

Na kama Fursa sio kubwa kama uwezo wako, unaweza kuitangaza biashara yako katika sehemu yenye fursa kubwa zaidi.

Hivyo ili kampuni ikuwe ni lazima vitu hivyo viwili kila siku viwe vinaongezeka na viende sambamba.

Na kanuni au fomula hii inatumika katika kila kitu  na si katika biashara pekee.

Natumaini utakuwa umejifunza kitu katika makala hii.

Kama una swali, maoni au ushauri comment chini na usisahau kuwashirikisha wengine ili na wao wanufaike na makala hii kwa kubonyeza vitufe vya mitandao ya kijamii vilivyopo hapo chini.

Ni mimi mwenye kujali mafanikio yako,

Dr. Said Said


Abdallah Hemedi
Abdallah Hemedi

Content Manager

Ujumbe Wa Facebook

Leave a Reply

Your email address will not be published.